Makonda: Vyombo vya Habari havitendei haki

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amevituhumu vyombo vya habari nchini kuwa vinadhoofisha maendeleo ya wananchi kwa kuminya haki yao ya kupata habari vikidhani vinamwadhibu yeye binafsi.
Makonda alitoa madai hayo jana Jijini Dar es Salaam wakati akihojiwa na Kituo cha Star TV kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo ya mkoa baada ya kutimiza mwaka mmoja. Alisema, baadhi ya vyombo vya habari vimepotoka kwa kumwadhibu yeye kwa madai ya kuminya uhuru wa vyombo hivyo baada ya kudaiwa kuvamia kituo cha Clouds Tv. Hata hivyo, alisema, hatua hiyo imegeuka kuwa adhabu kwa wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam kwani wanaokosa taarifa ni wao.
“Kama lengo ni kuniadhibu mimi wanakosea kwa sababu mimi kama Makonda, naandikwa sana. “Makonda aliwaambia watangazaji wa Star Tv katika mahojiano maalum mubashara. Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (MOAT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) vilitangaza kumfungia kuandika habari Makonda kwa madai alivamia kituo cha Clouds Tv akiwa na askari wenye silaha usiku na kuwatishia.
Hata hivyo, Makonda alisema, hakufanya uvamizi kama inavyodaiwa na waandishi bali alikwenda Clouds kama nyumbani kwa rafiki zake na kuwa madai hayo yametengenezwa ili kufifisha vita dhidi ya madawa ya kulevya. Alisema, kutokana na waandishi kumbania habari zinazohusu wananchi wake, wanakosa kujua maendeleo ya mkoa wao aliyofanya katika kilimo, ujenzi, miundombinu, afya.
Makonda hakuweza kufafanua zaidi juu ya alichokuwa ameandaa kama makala maalum ya mafanikio yake kwa mwaka mmoja sasa akiwa Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam. Makonda alisema alikuwa anamaliza kuandaa makala maalum ambayo ingerushwa katika vyombo mbalimbali vya habari na tayari baadhi ya vyombo vilishaanza kuiulizia viitoe.
Alisema makala hiyo haikuweza kutoka kufuatia kuzushiwa kuwa alivamia kituo cha Clouds TV na kisha kufungiwa na waandishi wa habari kutoa habari zinazohusu kazi yake. Ingawa hakuzama sana kuhusu suala la maendeleo, mpaka sasa amefanikiwa kujenga jengo la wodi ya kina mama Hospitali ya Mwananyamala, hospitali ya mama na mtoto iliyogharimu sh. bilioni 6 iliyojengwa kwa msaada wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Korea ya Kusini (KOICA) Chanika, wilayani Ilala na barabara ya simenti inayoelekea bandarini iliyojengwa na msamaria mmoja.
Pia Makonda alisema kwa kushirikiana na Clouds TV na vyombo vingine vya habari na wasanii, alifanikiwa kuendesha kampeni ya Jiji letu iliyolenga kuifanya Dar es Salaam ing’are. Alisema, masuala hayo ya maendeleo ndiyo ambayo habari zake hivi sasa wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam wanazikosa kwa madai kuwa anaadhibiwa yeye wakati siyo.
Alisema, vyombo vya habari vina dhamana ya kuwahabarisha wananchi na kuwajibika kwao hivyo ni makosa kuwanyima habari zinazowahusu. Mbali ya Makonda, hata Rais John Magufuli aliwahi kuvilaumu vyombo vya habari kwa hatua hiyo akishangaa vipi kukiwa na habari mbaya za Makonda zinaandikwa lakini nzuri haziandikwi kama kweli wameamua kumsusia.

Kuhusu madai ya elimu yake na kuhusihwa na jina la Daud Bashite, Makonda aliwataka wanaohoji wakaulize mamlaka za uteuzi ndio zinafahamu kwa kina historia ya elimu yake. Alisema anapigwa mawe na wabaya wake kwa sababu ya kubeba na kusimama ajenda ya kupambana na biashara ya dawa za kulevya

Comments