SERIKALI inafikiria kuunganisha taasisi zote zinazohusika na sekta ya uhifadhi wa wanyamapori nchini kuwa chombo kimoja chenye nguvu kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji wa taasisi hizo pamoja na kuongeza ufanisi wa kiutendaji katika sekta hiyo muhimu.
Akizungumza mwishoni mwa wiki bungeni mjini Dodoma wakati akihitimisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alisema anaunga mkono ushauri uliotolewa na wabunge mbalimbali ukiwemo wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Atashasta Nditiye juu ya umuhimu wa kuunganisha taasisi hizo za uhifadhi.
“Wakati umefika sasa, tusiwe na makampuni (taasisi) zaidi ya manne ndani ya sekta hii ya wanyamapori, tuwe na kampuni (taasisi) moja tu ambayo itapunguza gharama katika uendeshaji, tutaunganisha jeshi la wahifadhi na jeshi hilo tutakalolitengeneza ni jeshi moja tu ambalo litakuwa na malezi chini ya jeshi la wananchi wa Tanzania, ili kujenga nidhamu, kuheshimu haki za binadamu na kufanya kazi kwa mujibu wa maslahi ya taifa,” alisema Profesa Maghembe.
Aliongeza, “Jeshi hilo ambalo tunaliandaa kisasa, jeshi usu litakuwa na ‘chain ya command’ moja na litawajibika kijeshi kwa makosa ya haki za kibinadamu na usaliti wa taifa au usaliti wa uchumi wa nchi yetu.” Awali akiwasilisha bungeni hotuba ya bajeti ya wizara yake, Profesa Maghembe alizitaja taasisi hizo kuwa ni Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (Tawa) na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (Tawiri).
Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) lilianzishwa mwaka 1959 kwa Sheria ya Hifadhi za Taifa Sura 282 na kupewa dhamana ya kusimamia na kuendeleza maeneo yaliyoanzishwa kisheria kuwa Hifadhi za Taifa. Hifadhi hizo ambazo zipo 16 zina jumla ya kilometa za mraba 57,365.80.
Kwa upande wake, NCAA ilianzishwa kwa sheria na kupewa jukumu la kusimamia eneo la kilometa za mraba 8,292 kwa ajili ya kuhifadhi, kuendeleza utalii na wafugaji wenyeji wa eneo hilo ambapo wakati ikianzishwa walikuwa takriban 8,000 mwaka 1959 na idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia zaidi ya wakazi 90,000 mwaka jana.
Comments
Post a Comment